KOCHA
wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars), Mbrazili, Marcio Barcellos
Maximo, amesema yuko tayari kuchukua nafasi ya Hans van Der Pluijm na
kuinoa Yanga.
Maximo, 52, amesema anachotaka ni ofa nzuri ili aje nchini kuinoa
Yanga kwa kuwa sasa mkataba wake na kikosi cha Fracana unakwenda
ukingoni na yuko huru.
Habari za uhakika kabisa kwa asilimia kubwa, Maximo akishirikiana na
mwakilishi wake hapa nchini, amefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Yanga,
Yusuf Manji na wamefikia makubaliano kwa zaidi ya asilimia 90.“Kweli kumekuwa na mazungumzo kati ya Manji na Maximo, kocha amekubali kuja na hata mwakilishi wake amethibitisha hilo.
“Unajua mwanzo kocha alikuwa na mkataba na timu yake kule Brazil, sasa
mwenyekiti akamuwekea ngumu na suala la kuvunja mkataba likaingia kuwa
na fedha nyingi sana ili uvunjwe, Yanga wakashindwa.
“Lakini safari
hii nimezungumza naye na kaniambia yuko tayari kuja, ameishafanya
mazungumzo na Manji kuhusiana na kuja kwake na amekubali,” kilieleza
chanzo cha uhakika.
“Safari hii ni tofauti kabisa na ilivyokuwa
awali, Maximo yuko tayari kuja na yuko huru. Ameniambia anataka kuja
kuifundisha Yanga,” kiliongeza chanzo.
Juhudi za kumpata Manji kwa siku mbili hizi zilifanikiwa lakini
alisema yuko nje ya nchi kikazi, alipoulizwa kuhusiana na suala la
Maximo, akasema atajibu baada ya kurudi nchini baada ya siku mbili.
Championi: Lakini tungependa kujua kuhusu suala la Maximo.
Manji: Mnaonaje mkisubiri nitakaporejea baada ya siku chache?Pamoja na kufanya mazungumzo na Maximo, Yanga imeendelea kufanya
mazungumzo na makocha wengine kupitia msaada wa Pluijm ambaye pia
anawatafutia wachezaji. Iwapo watashindwa dau la Mbrazili huyo tena,
basi watachukua kocha atakayependekeza.
Maximo aliiwezesha Tanzania
kucheza michuano ya Afrika tangu mwaka 1980 ilipocheza Kombe la Mataifa
Afrika baada ya kuivusha Taifa Stars hadi katika michuano ya Chan
nchini Ivory Coast lakini ikatolewa na Zambia hatua ya makundi.
Maximo alikuwa kati ya makocha waliokuwa wanatakiwa kuinoa Yanga miaka
miwili iliyopita, lakini ikashindikana baada ya mwenyekiti wa timu
anayoifundisha kuweka ngumu na Yanga ikamtwaa Mbelgiji, Tom Saintfiet.
Championi: Sawa, lakini angalau tujue kama kweli mmezungumza na Maximo.
Manji:
Ok, tumewasiliana, lakini si wakati wa kusema tumewasiliana kuhusu
nini. Kweli inawezekana ni masuala ya mpira au mambo binafsi.
Taarifa nyingine zinasema Maximo ameshaanika dau lake na yuko tayari kuja kama Yanga watampatia anachokitaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni