Maskini! Wakati tasnia ya filamu Bongo ikiwa katika majonzi ya kuondokewa na ‘dairekta’ na mwigizaji mkubwa, Adam Phillip Kuambiana (38), pigo lingine limetokea kwa wasanii hao kwa kuondokewa na kichwa kingine, Sheila Haule ‘Recho’ (26).Recho alikutwa na umauti Mei 26, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar alipokuwa amelazwa baada ya kujifungua kwa oparesheni Mei 25, mwaka huu kwenye Hospitali ya Lugalo, Dar.
KUJIFUNGUA
Kwa mujibu wa chanzo makini kilichokuwepo kwenye Hospitali ya Lugalo, Recho alikuwa akisumbuliwa na tatizo la presha ya kupanda, kisukari na kifafa cha mimba.
Chanzo hicho kilieleza kuwa, kwa zaidi ya saa 23 tangu afikishwe hospitalini hapo, Recho aliteseka kwani madaktari walikuwa wakihangaika kuishusha presha ili kuweza kunusuru uhai wake hivyo staa huyo alipigania uhai wake kwa masikitiko makubwa.
“Tulipomfikisha alifanyiwa vipimo, ikagundulika ana tatizo la presha na kisukari na hata alipojifungua alipata kifafa cha mimba ndipo hali ilipozidi kuwa mbaya,” kilisema chanzo hicho kilichoomba hifadhi ya jina.
UTABIRI WA KUAMBIANA
Chanzo hicho kilizidi kueleza kuwa, pamoja na jitihada za madaktari kuhakikisha wanaokoa maisha ya mwigizaji huyo na mwanaye, walifanikiwa kumfanyia oparesheni, mtoto wa kiume akatoka salama lakini muda mchache baadaye alifariki dunia huku Recho akiwa katika hali mbaya.
Kwenye gazeti la Amani lililopita toleo namba 814 la Mei 22, mwaka huu, kulikuwa na habari iliyomhusu Recho juu ya marehemu Kuambiana aliyemtabiria kuwa atajifungua mtoto wa kiume iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka: “Kuambiana alimtabiria mtoto Recho”.
Katika habari hiyo, Recho alieleza namna alivyokutana na Kuambiana na kumtabiria kuwa atajifungua mtoto wa kikume, kweli ikatimia kwani alijifungua mtoto huyo lakini bahati mbaya alifariki dunia hivyo kuacha huzuni kubwa.
Utabiri huo ulipotimia Jumapili iliyopita, uliibua simanzi nzito kwa baadhi ya wasanii hasa baada ya mtoto kufariki dunia huku wengi wao wakikumbuka utabiri alioutoa Kuambiana.
KUHAMISHIWA MUHIMBILI
Baada ya madaktari wa Lugalo kuona tatizo linazidi, Jumatatu iliyopita walilazimika kumhamisha Recho katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
“Ilibidi apewe ‘transfer’ ya kwenda Muhimbili kwani hali yake haikuwa nzuri hasa baada ya kujifungua na kupata kifafa cha mimba, akalazwa ICU,” kilisema chanzo hicho.
MADAKTARI WAMFICHA MCHUMBA’KE
Taarifa kutoka Muhimbili zilidai kwamba baada ya kuona umati wa wasanii wa Bongo Movies usiku hospitalini hapo, madaktari walilazimika kumficha mchumba wake, George Saguda pamoja na wasanii wengine kwani walitambua pigo walilolipata hivi karibuni kwa kuondokewa na mwigizaji Kuambiana.
“Waliona watawaongezea majonzi kwa kuwapa taarifa za msiba hivyo wakalazimika kuwaficha hadi Jumanne asubuhi ndipo wakatoa taarifa za kifo,” alisema nesi mmoja wa Muhimbili bila kutaja jina.
ODAMA ABAKI NA SIRI NZITO
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa Recho na shosti yake kipenzi, Jennifer Kyaka ‘Odama’ wawili hao walikuwa watu wa karibu mno.
Ilielezwa kwamba Recho na Odama walikuwa wakishirikiana kwa kila jambo hivyo atakuwa amebaki na siri nzito Recho.
“Marehemu amemuachia siri nzito sana Odama, walikuwa wakishirikiana katika kila kitu na kutunziana siri nyingi nje ya kazi ya sanaa,” kilisema chanzo hicho.
Recho alilelewa na bibi yake baada ya kufiwa na wazazi wake wote hivyo mipango ya kumsafirisha marehemu iliendelea kufanyika juzi Jumanne ambapo wasanii walitarajia kuchangisha shilingi milioni kumi kufanikisha shughuli ya kuaga, majeneza (mama na mtoto) na kusafarisha msiba kwenda nyumbani kwao Songea, leo Alhamisi.
Mpaka Recho anapatwa na umauti, alikuwa akijulikana zaidi kwa jina la Rachel Haule lakini kwa mujibu wa mama yake mdogo ambaye jina halikupatikana, marehemu alibatizwa kwa jina la Sheila Haule.
Recho aliyezaliwa 1988, aliingia kwenye fani ya uigizaji mwaka 2009. Baadhi ya filamu alizocheza ni pamoja na Loreen, Unpredictable, Danger Zone, Men’s Day Out, Vanessa (yak wake mwenyewe na nyingine. Fuata makala ukurasa wa 9. Sisi wote tu mavumbi, mavumbini tutarejea. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni